Tuesday, January 17, 2006

MKO WAPI WANAMAPINZUZI NA WASOMI WETU?

“ Kama ningekuwa kijana ningeanzisha Mapinduzi “ aliongea Mzee wa mika 80. “Mapinduzi ya nini?niliuliza” ya kila kitu “ alijibu .
Watanzania walio wengi watakubaliana na mzee huyu kwa sababu katia ya watanzania watatu ( 3 ) unaokutana nao wawili (2) wanakiri kuwa kuna umuhimu wa kufanyika mabadiliko. Kama umma unapigania marekebisho yafanyike, mara nyingi wanapigania mabadiliko kwenye elimu, Afya, Kilimo, Maji, Sheria na Sera za kiuchumi. Katika nchi watu wanapingana dhidi ya ujinga , umasikini na maradhi lazima pawepo na kilio cha mabadiliko.
Katika nchi yeyote Duniani panakiwepo na Biashara isiyo na usawa , mamlaka ya sheria kutotoa haki , huduma mbaya za mahospitalini, Elimu yenye ubaguzi unyanyasaji wa kijinsia pamoja na ubaguzi wa kidini , kikabila na uchafuzi wa mazingira, yote haya yamewaacha watanzania wakilalamika .
Sasa tujiulize tufanye nini? Biblia inatambua “ Mtawatambua kwa matunda yao. Je Watu huchuma zabibu katika miiba au tini katika mibaruti? Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri na mti mwovu huzaa matunda mabaya. Mti mwema hauwezi kuzaa matunza mabaya wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri. Mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni. Ndipo kwa matunda yao mtawatambua” Mt: 7:16-20 .
Kwa mtazamo huo huo, hata tukihubiri matatizo yaliyosababishwa na rushwa, watu kunyimwa haki zao za kimsingi , umaskini uliokithiri, uharibifu wa mazingira na mabo mengine. Mizizi yake ni mrefu zaidi kuliko tunavyofikiria. Kinachihitajika ni mabadiliko ya mfumo mzima. Tunahitaji Serikali itakayoleta mfumo mpya wa Kuongoza na kusimamia vizuri rasilimali za Taifa. Serikali itakayowapa wananchi Elimu bora, kazi , Nyumba, Chakula ( Kilimo chenye ruzuku ) Hospital zenye madwa na kuhifadhi mazingira.
Upande mwingie wa pili, kma kweli tunahitaji mabadiliko ya kweli ya kuwa na nchi isiyokuwa na rushwa , serikali isiyokuwa na matatizo niliyoeleza , ni lazima sisi wananchi tuwe tayari kubalika na si tu serikali ibadilike.Je Nauliza ni vijana wangapi wako tayari kubadilika? Na uliza Vijana. Tunapaswa kuwacha kuendelea kumlaumu Mungu, Kwa viongozi wabaya eti ni chaguo la Mungu, sisemi Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Serikali yake ni viongozi wabaya la asha lakini kuna viongozi wengine waliochaguliwa kwa mkumbo wa chama ambao hawafai na wananchi wanawafahamu, Matokeo yake watampa shida Mheshimiwa Rais.
Embu fikiria kwa mfano, mti uanguke Mtu afe, watu watasema ni mapenzi ya Mungu , Je Mungu, ndo aliyesababisha Mti uanguke? Lazima tujiepushe na malalamiko ya kuwa Mungu anapenda tupate shida au anatujaribu, sio kweli matendo mengine ni matendo ya watu . Umeingia ugonjwa unaoitwa kwa kiingereza “Mind your own Business” Je lipi halikuhusu unataka kusema mali ya Umma haikuhusu? Kama kwili inakuhusu kwanini unaka kumya? Lakini hii imekuwa ni tabia ya watanzania make kila mmoja anaogopa kuitwa adui wa umma ebu fikilia kama tunaangalai mabibi zetu wanawatahiri watoto wa kike ili wawaongezee soko kwenye soko la ndoa, watoto wadogo wanaingizwa kwenye biashara ya mapenzi, tunakaa kimwa,kwa sababu ya ugonjwa wa “mind your own business’’,ni ugongwa kwa sababu unawafanya watu wanaumwa matokeo yake mtu akifa kutokana na matendo hayo yote, tunasema ni mapenzi ya mungu.Huku ni kufanana na Yuda Iskarioti na vipande thelathini 30 vya fedha.
Hakuna kitu chochote kisichowezekana lazima tuwe tayari na tujiandae kubadilika,lazima kwanza tubadilishe fikra zetu,na hii itachukuwa muda ,lazima tuondokane na zana haiwezekani kwenda inawezekana,haifanyiki kwenda inafanyika siko tayari kwenda niko tayari ili mradi yawe yanaleta mabadiliko katika nchi.Lakini tukumbuke mabadiliko yatakuja jinsi utakavyo jiandaa! Msemo wa wanafarisafa kwamba aliwazalo mjinga ndilo litakalo mtokea. Ukitaka kujua mabadiliko ya gafla yataiharibu jamii na mabadiliko ya taratibu sana yataidumaza jamii.Kabla ya Marekani na Wingereza kufikia hapa walipo ilichukuwa kipindi kirefu. Nina uhakika na sisi tutafika hapo siku moja. Lakini lazima tuanze kuwa na siasa za uvumilivu, siasa za kuwavumilia wenye mawazo tofauti na sisi, hasa mawazo ya kisiasa lazima tuvunje ukabila unaoanza kujitokeza kwa sasa ili tuweze kuendelea kiuchumi.Usiniulize kwa nini dini imeshindwa kutuunganisha? narudia madiliko yeyote ya yanachukuwa kipindi kirefu lakini tunaweza kuanza taratibu kuwachanganya watoto kutoka kwenye tabaka mbalimbali shule moja, kuwashawishi wafanya biashara kuwa wajasilimali ilikutoa ajira.
Yote haya yanahitaji mabadiliko kwenye siasa na sayansi, ilikubadilisha mfumo mzima wakijamii na kiuchumi ilituweze kutoka kwenye mfumo wa jana mpaka mfumo wa leo,kubadilisha fukra kutoka kwenye mtu mwenye kitambi na gari la kifahari kwenda kwenye mtu mwenye upeo wa mambo.Tusiwalaumu sana wazee wetu kwa hayo,kwasababu program wanayotumia ilifanikiwa katika miaka 1980 ya plan” A”.
Tukirudi nyuma tukatazama upande mwingine tunawaona vijana wengi tu na wasomi wako serikarini jiulize yako wapi mabadiliko?ziko wapi fikra na mawazo mapya ya kiuchumi na kijamii?Au hayawahusu!! “Non of their Business” ugonjwa usio na tiba. Uko wapi uwekezaji kwenye taharuma, teknolojia na uzalishaji kwa ajili ya Umma, mambo yatakayotusaidia kukuza Uchumi wa kesho? Ni nani wa kuanzisha Agenda hii? Nani anataka kuitwa adui wa Umma?
Labda tusiwalaumu wanaweza kuonekana ni vijana, kwa mavazi ya ujana kama mimi,lakini wakawa na mawazo yaliyofanya kazi miaka 1980, miaka ya plan “A” . Jiulize wako wapi viongozi wa kutuongoza kwenye Karne ya 21 au labda hawajazaliwa kwa nini hivi? Ukiwauliza vijana kwanini hawako msitari wa mbele kwenye uongozi na katika mabadiliko ya sera za Kiuchumi, Kisiasa na Kijamii! Wataguna ! Hatuwezeshwi” wazee hawatutaki vijana. Au hatujapata mtu wa kutuwezesha. Vijana kuwezeshwa ni sababu za kimsingi ya kusubiri? .Mahatma Gandhi alipojitokeza kwenye Siasa za India wakati Aridhi ikiwa chini ya Falme na milki za Kikoloni, je yeye alipata uwezeshwaje upi? Nani aliyemchangia pesa au nani alimpa msaada wa Kampeni? Au Nelson Mandela alipoanza kupambana na Tawala wa ubaguzi wa rangi mpaka akawakomboa wazalendo wa Africa ya Kusini nakuwaletea Uhuru ni nani alikuwepo kumwezesha au aliwezeshwa na nani au ni msaada gain walioupata wapigania Uhuru wetu walipoingia misutuni? Mbali na kutopata msaada waliishia Jela na Vizuizini na kutangazwa wasaliti hata kwa Jamii zao wenyewe.
Hebu niishie hapa, tunaishi kwenye nchi yenye Demokrasia, yenye Uhuru wa kuongea na Uhuru wa vyombo vya habari. Niliposema wakati wa Mapinduzi ni sasa sikuimanisha na wala sitaimanisha kwamba kila Kijana achukue jiwe aponde Vioo vya Magari barabarani au tuandamane Barabarani, siyo hivyo, na hivyo si maana yangu na wala hata siku moja sitaimanisha hivyo. Na kama kuna mtu mwenye fikra kama hizo ni mtu nwenye akili finyu na niwakubezwa ni mtu asiyetufaa katika Jamii ya sasa. Lazima vijana na tuwe na sera za mabadiliko ya Kiuchumi naya Kisayansi, lazima tujitokeze kupigania nafasi mbali mbali. Ingawa uchaguzi umeisha lakini tunacho cha kutusaidia au tunae mheshimiwa Rais upande wetu tusife moyo.La pili mwaka 2007 ni mwaka wa uchaguzi mkuu ndani ya chama cha mapinduzi{ccm}na kwa kadirio la chini kila penye watanzania watatu{3} wawili{2}watakuwa na umri chini ya miaka 40.Je tuna sera zipi za kuwapa watuchague ili tushike uongozi wa juu ndani ya chama?Je tuko tayari kuwa na mawazo ya mapinduzi ya kisiasa na kiuchumi?Amkeni wakati wa ukombozi ni huu!!

Wednesday, January 11, 2006

UMASKINI WETU NANI ALAUMIWE?

Je kuna njia ya Mkato katika Maendeleo ya Kiuchumi ya Tanzania?. Swali hili limezua mjadala mkubwa kwa miongo mingi. Mjadala huu umewaingiza wahazili wa vyuo, wachumi wa kimataifa, umoja wa Mataifa na Vitengo vyake vya uchumi, Umoja wa Africa ( Au), wanazuo na viongozi wa dini. Maazimio mengi yamewekwa , Ripoti mbalimbali zimewekwa. Matokeo yake yamekuwa ni sawa na bure, Huku nchi za Africa, Tanzania ikiwa ni miongoni zimebakia kuwa maskini wa kutupwa cha kutisha zaidi hali inaendelea kuwa ngumu.
Mpaka sasa maswali mengi ya kiuchumi bado hayajajibiwa, ingawa tunaambiwa uchumi wa nchi unakua. Je tutaendelea kupokea maelezo hayohayo au kuna njia nyingine? Au tuendelee kuziona nchi za magharibi kama Mungu wa pili? Kwa sababu wakati Watanzania tunazidi kulia na kupigana na umasikini, Nchi za magharibi zinazidi kung’ara machoni mwa watanzania kuanzia kwa viongozi mpaka kwa mwananchi wa kawaida. Na sasa tunawaona kama watu wema, wa mcha Mungu wanaosamehe watu madeni yao, wanaotoa msaada wa nguo kwa masikini, watu wanaowaangalia watoto yatima na wajane, watu wanaopenda maendeleo ya Watanzania, watu waliotuletea demokrasia na sifa nyinginyingi tu ambazo mpambe wa mwenye Mgodi Mererani angependa amsifie bosi wake pindi shimo lake likitoa madini. Matokeo yake ni watanzania kuendelea kuchezea matapishi yetu wenyewe.
Ebujiulize lipi limeenda kombo? Je ni urithi tuliorithi kwa maendeleo hafifu au viongozi wetu? Waza maswali mengi tu ujiulize na kwanini sisi na siyo wao? Slogan mbalimbali zimetawala medali za siasa na uchumi kama “saa ya ukombozi ni sasa” Ujamaa na kujitegemea “Haki sawa kwa wote:” Mageuzi na umoja “ Uchumi wa soko huria” Yako wapi matokeo yake kwa mwananchi wa kawaida?
Hebu tujiulize tutaendelea na majaribio haya au ndiyo tunajaribu njia nyingine ya mkato? Hili ni swali ambalo kila mtanzania anapaswa kujiuliza, nasema kila mtanzania ajiulize kwasababu Maendeleo ya Kiuchumi au Kisiasa hayataletwa na mtu mmoja, ni ya watanzania wote kwa pamoja. Baba wa Taifa hayati Mwl Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema kwamba “ aliwapeleka wamasai shuleni kwa FFU, waliporudi nyumbani wakati wa likizo, hakuna aliyerudi shuleni tena” hayo yalikuwa ya wamasai sasa tunaendelea kushuhudia kabila la wahazabe wakikataa kutoka porini lakini viongozi hilo hawalizungumzii. Chakushangaza tumezidi kukaa kimya wakati watoto wa kike wakiendelea kutahiriwa ili kuwaongezea soko la ndoa , Jamii ya watoto yatima ikibaguliwa, wajane wakinyang’anywa mali walizochuma na Waume zao enzi za uhai wao,tukizidi kuwanyanyapaa wagonjwa wa ukimwi. Maofisini nako Ugonjwa wa njoo kesho na rushwa vikikosa tiba na kuendelea kuwa kero kwa Mtanzania, Kufungua Kampuni kwa Mtanzania huchukua siku mia ishirini na tisa (129) wakati kwa mgeni ni siku ishirini na tisa ( 29 ) Kazi maofisini hupatikana kwa vigezo vya kumfahamu mtu na si mtu anajua nini . Uporaji wa mali ya nchi kuitwa uwekezaji , cha kushangaza hawa wawekezaji wameingia mpaka kwenye biashara ambazo watanzania wanaziweza.
Leo hii nenda Kariakoo utawakuta wachina wana maduka ya nguo za mtumba, maduka ya vyombo vya jikoni,jiulize wapemba na wachaga hawapo wakuendesha hayo maduka, nasikia eti kuna wawekezaji kwenye kuuza karanga pembeni mwa barabara kutoka nje ya nchi. Ili kufahamu ya leo lazima utazame ya nyuma na kufahamu ya mbele lazima tuangalie ya nyuma na ya leo, hii ni kwa njia ya kisayansi.Tunaambiwa umaskini wetu umesababishwa na umaskini wetu,falsafa ya mmarekani mmoja ya “vicious circle of poverty”kulifunga duara hili kufuatana na maelezo yake tunahitaji wawekezaji wa nje{foreign investment}Wakati ni sahihi kuwa uwekezaji huo ndio umetufanya tuwe maskini.
Wanafalsafa wanaamini kuwa hakuna kinachotokea katika maisha ya binadamu leo ambacho ni kipya.Wanaamini kuwa kila kinachotokea leo ama kimeandikwa kwenye misaafu mbalimbali ya dini au kilitabiriwa na mababu zetu miongo kadhaa iliyopita.
Hebu tujiulize hatuko maskini sasa kwa sababu ya ukoloni?kwa njia moja au nyingine tumetawaliwa na bado tunaendelea kutawaliwa kifikra mpaka leo{ukoloni mamboleo}.Si ukoloni uleule ulioleta uwekezaji wa nje?mbona bado tuko maskini?Jiulize itakuwaje leo utukomboe kutoka kwenye umaskini?Ni kweli na itaendelea kuwa kweli kwamba uwekezaji wa nje hauwezi kutusaidia kujikwamua na umasikini kwa misingi ya kila mwananchi kunufaika, Kwa mtindo huu wa makampuni haya kuchukua faida kubwa nje ya nchi. Matokeo yake ni pengo la wenye nacho nawalala hoi kuzidi kuongezeka kwa kasi ya kutisha kila kukicha. Huku sera zetu zingiendelea kusisitiza uzalishaji kwa ajili ya soko la nje ( Soko la dunia ) au soko huria ambalo mnunuzi ndiye anayepanga bei na si muuzaji. Tunavyozidi kuzalisha kwa ajili ya soko hilo, (soko la dunia) ndivyo tunavyozidi kusahau au kupiga kumbo uzalishaji kwa ajili ya watu wetu na maendeleo yao.
Chukua mfano wa nchi za Korea ya kaskazini, Botswana, China, na Albania hizi nchi zote zilikuwa maskini kama sisi lakini wao waliamua kuachana na Mfumo wa Bank ya Dunia, IMF, na soko la dunia kwa kufuata uchumi wa kijamii wa Kuzalisha kwa ajili ya watu wao na maendeleo yao ya kiuchumi , matokeo yake mataifa ya nje yamewafuata ili wawauzie bidhaa zao kwa bei inayopangwa na muuzaji na sio bei ya mnunuzi.
Jiulize tena na tena umasikini wetu nani alaumiwe? Kwa kuuliza swali kwa njia hii ni rahisi kuona kwa kupitia kwenye kioo, kipi kilichosababisha tuwe masikini wakati nchi ni tajiri?Ingawa nimeandika sintashangaa kusikia mtu au kundi la watu wenye msimamo wa soko huria ,soko la dunia na muongozo wa Benki ya dunia,wakinibeza,kwa kuuliza swali hilo,kwa sababu mafundisho na maelekezo yao yanamuangalia mtu au kundi la namna ya kwangu kama mtenda maovu na Adui wa umma.Ebu endelea kujiuliza kama Mmarekani au mwingereza anayekaa New York au London kupanga maendeleo ya Mtwara au Lindi?Ambako hajawahi kufika.Jiulize tena na tena .
Nina matarajio mengi kutoka katika serekali ya awamu ya nne ya mheshimiwa Jakaya Kikwete.Mheshimiwa Rais anaonekana kuwa ni mtu wa watu na mpenda maendeleo ya watanzania walio wengi.Nasema hayo kwa sababu ni kiongozi wanchi ambaye watoto wake wamesomea na wanasomea Tanzania.Huo ni mfano mzuri wa kuigwa na viongozi wengine, na hii inaonyesha ni jinsi gani mheshimiwa Rais alivyo na imani na elimu ya kitanzania inayomfundisha mtanzania kuwa mtanzania kila sehemu alipo. Hotuba yake ya bungeni inaongeza matumaini yangu kwa kweli. Na kumuona kama mtu anayeweza kubadilisha mkondo wa uzalishaji kutoka kuzalisha kwa ajili ya soko la dunia kwenda katika uzalishaji kwa ajili ya wananchi, kubadilisha sera za uwekezaji kutoka kutegemea uwekezaji wa nje kwenda katika uwekezaji wa ndani. Wakati huhuo na sisi wananchi tuwe tayari kumuunga mkono kwani maendeleo yetu hayataletwa na Rais tu bali na sisi wanachi tuwe tayari kubadilika.
Wakati wa ukombozi ni huu tusisubiri mtu wa kupeleka watoto shule kwa FFU ni jukumu letu sisi wote kufanya kazi kwa Ari mpya, Kasi mpya na nguvu mpya. Je tunao uwezo wa kufanya maamuzi yetu wenyewe? Kama tunao Mungu Ibariki Tanzania ,Mungu mbariki Mheshimiwa Jakaya Kikwete.