Tuesday, May 23, 2006

SUALA LA KATIBA TANZANIA LITAZAMWE UPYA

Katika nchi yeyote duniani inayofuata misingi ya Kidemokrasia,Katiba ni chombo kinachotoa muongozo mkuu wa kuhakikisha Demokrasia inakuwepo nchini.Katiba ndio msingi wa Uongozi bora na muhimili wa Serikali,pia ndio muongozo wa Taifa,na mtetezi wa haki za binadamu Kitaifa na Kimataifa.
Nimesema suala la Katiba Tanzania litazamwe upya kwa sababu zifuatazo na za msingi:Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikilalamikiwa si na Viongozi wa vyama vya upinzani bali na wadau mbalimbali wa haki za binadamu na watetezi wa Demoklasia. Suala la Katiba sio tu kwamba lilikuwa likiibuka kwenye vyombo vya habari tu bali hata kwenye vyomba vya sheria kama vile Mahakama kuu. Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inasemekana kuwa na mapungufu mengi, na cha msingi zaidi ni kwamba Katiba hii ilitungwe\kuandikwa chini ya chama kimoja.

Katika mapungufu haya ya Katiba,Serikali imekuwa ikifanyia marekebisho. Marekebisho haya mimi nayaona kama kuichezea Katiba ya nchi,katika hili la marekebisho Serikali imekuwa inaamini na kuufanyia kazi msemo au methali ya usipoziba ufa utajenga ukuta, lakini wamekuwa wakishindwa kuelewa kuwa ufa huu ni mkubwa na umetokea kwa sababu nyumba hii imejengwa kwa matofali ya udongo,huku wao wakijaribu kuziba ufa huo kwa kutuma matofali ya sementi. Matokeo yake nyumba imelemewa na sasa inakaribia kuanguka yote, baada ya matofali ya sementi kuyazidi nguvu matofali ya udongo na msingi wake. Nini kifanyike kabla nyumba hii ijabomoka wakati wa kipindi cha masika?cha kufanya ni kuitisha mchango (mchakato) wa Kitaifa kuchangia nyumba mpya (Katiba mpya) itakayo jengwa pembeni au mbali kabisa na nyumba hii (Katiba hii) ya sasa.

Hapa kuna mambo ya msingi ya kuzingatia wakati wa mjadala huu wa kitaifa kuhusu katiba ya nchi,suala la msingi ni kutowaruhusu wanasiasa waichezee Katiba hii kwa kuongeza muda wao wa kukaa madarakani kama ambavyo tumezoea kusikia nchi mabalimbali za Africa zikifanya.Juzi Nageria wameshindwa kufanya hivyo.Uganda ilifanikiwa na kumuwezesha Museven kugombea tena, kwa kisingizio eti bado anapendwa na wananchi wa Uganda.Hapa ngoja niwafafanulie, viongozi wa Africa kuwa kupendwa kwao na wananchi hakutokani na mambo mema waliofanyiwa na viongozi wao, ila kunatokana na wananchi kuwaogopa viongozi wao pindi wakitoka madarakani wasije wakaanzisha fujo,Hali hii kisoikolojia tunaita nidhamu ya woga. Na nidhamu hii imeendelea katika nchi zitu za Afrika huku viongozi wakijivunia kupendwa na wananchi, wakisahau msemo wa kwenye Biblia wa kuzisoma Alama za nyakati na kuzielewa. Matokeo yake tumewaona viongozi wakijigamba kuwa wameleta na kuimarisha amani kwenye nchi zao. Kitu ambacho sio cha kweli huwezi kusema nchi yako ina imani wakati ndani ya nchi yako kuna wananchi wanaokufa kwa njaa au watakula nini mchana. Hivyo sio nchi ya amani ila ni nchi yenye wananchi waoga ambao wametulia kama maji kwenye mtungi ambao ukipata mtu wa kuutingisha mtungi huo huchukua muda kutulia.
Hii ni sawa na nchi zetu zile zinasemekana kuwa na amani,zikipata watu wachache wa kuwashawishi wananchi na kuanza vurugu au vita huchukua muda mrefu kupata amani mfano mzuri ni Ivory cost,Nchi iliyokuwa inachukuliwa kuwa nchi ya amani kule magharibi mwa Afrika,Angalia kwa sasa machafuko yalivyo. Na haya yanaweza kutokea Tanzania kama maoni ya wananchi na wadau mbalimbali wapenda amani na Demoklasia ya kutunga Katiba mpya ya nchi yatapuuzwa.

Mfano mzuri ni Zanzibar,tumeona na kusikia wanzibar kumi wameenda Mahakamani kudai hati ya mkataba wa Muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika, sasa kama ungeitishwa mjadala wa Kitaifa kuhusu Katiba suala hili lisingeenda Mahakamani badala yake lingeongelewa na kujadiliwa na wananchi wa pande zote za Muungano Zanzibar na Tanganyika, mategemeo yangu kuwa matakwa au maelezo ya hawa watu wangeyapata kutoka kwa wananchi.
Nimesema suala la Katiba litazamwe upya kwa sababu nyingi tu ingawa nyingine nimeishazitaja lakini kuna nyingine. Katiba hii tuliyonayo inatoa mianya kwa Serikali zetu.zote mbili ya muungano na Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar.Kuichezeachezea au kuigombania kama mpira wa kona. Mwaka jana tuliona waziwazi uvunjaji wa Katiba hii pale Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilipoamua kuwa na Bendera yao, ambayo mpaka sasa hivi inatumika Kimataifa, Hapa kwenye michezo, tumeiona Bendera hiyo ikibebwa na Timu ya Polisi Zanzibar. Hapa ndio tunaweza kuanza kusema sasa Tanzania Visiwani ina uhuru wa Bendera,kama sio hivyo basi tukubali na kukili kuwa Zanzibar kuwa na Bendera yake ni uvunjaji wa Katiba.
Nasema haya yote kwa masikitiko na kwa mshangao kwa sababu kipindi chote cha miaka 40 ya Muungano hakuna aliyetegemea au kutarajia tukio kama hili la Bendera ya Zanzibar, wote tuliamini kuwa Bendera zote za Zanzibar na Tanganyika zilizikwa mnomo 26\4\1964. Tangia hapo tumekuwa tukiamini kuwa Tanzania ni nchi moja na ni Jamuhuri ya Muungano.Angalia Katiba ya nchi Ibada ya kwanza naya pili “ Tunaposema Jamuhuri ya Muungano, Tunaimarisha eneo lote la Tanzania bara na la Tanzania Visiwani. “Hivi Zanzibar ikiamua kuwa na wimbo wake kuna mtu atahoji?Au akitokea kikundi cha watu au mtu akadai kuwa na Bendera ya Tanganyika kwa kutumia vigezo vilivyotumiwa na Serikali ya Zanzibar kuwa na Bendera yake tutasemaje? Au tutaenda Mahakamani au hicho kikundi tutakiweka kizuizini. Kama Zanzibar imekuwa na Bendera yake iko wapi Bendera ya Tanganyika? Na itakuwa wapi Bendera ya Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania?
Siku chache zilizopita Mahakama kuu ilitoa uamuzi wa kutaka baadhi ya vifungu kwenye Katiba vifutwe,ikidai mhimili huo wa dola umepewa mamlaka hayo Kikatiba. Sasa nashangaa kama Katiba ndio yenye mamlaka makubwa kwenye nchi je Mahakama itakuwaje na uwezo wa kufuta baadhi ya vipengele kwenye Katiba, kama Katiba ndio mama wa Taifa. Mtoto wa mama huyu hamkosoe mama yake hadharani au aseme mama anamakosa kabla ya mme wake (Serikali na wananchi) ajaona hayo makosa. Au labda mme wake ameyaona ila kwa sababu mke wake ni mzuri anaogopa kumkemea.Uamuzi wa Mahakama kuu wa kuagiza kufutwa kipengele kinachowalazimisha watu kugombea nafasi za uongozi kwa kupitia nyama vya siasa. Na kuagiza kila mtu aruhusiwe kugombea nafasi za Uongozi kwa kupitia chama chochote, Mahakama kuu katika maamuzi yake imeamua kuwa ni haki ya kimsingi naya kila raia kugombea Uongozi ndani ya nchi bila kulazimishwa kujiunga na chama chochote cha Kisiasa. Mahakama kuu imetoa ukumu hii kulingana na haki za binadamu na kutokana na Katiba hiyohiyo,Inayokatazwa kuwepo kifungu chochote ndani ya Katiba kinachopokonya haki mwananchi iliyo katika Katiba.
Inaonekana hukumu hii ya Mahakama utaadhiri sheria nyinginezo, sasa ili kulizuia jambo la msingi ni kuhitishwa mjadala wa Taifa nchi nzima badala ya Serikali kukimbilia kukata rufaa kwa sababu kama Katiba imeipa uamuzi huo kwa kuzingatia Ibara ya 30 kifungua cha 3 kinachosema: Mtu yeyote anayedai kuwa sharti lolote katika sehemu hii ya sura hii au katika sheria yeyote inayohusu haki yake au wajibu wake, limevunjwa, linavunjwa au inaelekea ilitavunjwa na mtu yeyote popote katika Jamhuri ya Muungano anaweza kufungua shauri katika Mahakama kuu. “sasa kwa msingi huu ni bora suala hili la Katiba ya Jamhuri ya Muungano litazamwe upya na wadau wote wenye mamlaka ya kufanya hivyo chini ya Katiba.

Thursday, May 18, 2006

UTUMWA ULIOKITHIRI KWENYE MASHAMBA YA MAUA- ARUSHA

Mazingira machafu ya kazi,kazi isiyo na dhamana,kazi za kulazimishwa,ubabe wa kupita kiasi kutoka kwa wamiliki wa mashamba hayo,na kuishi maisha ya samaki,ni maisha ya kawaida kwenye mashamba makubwa ya maua –kanda kazikazini,hasa Arusha (Geneve ya Africa) Wafanyakazi ndani ya mashamba haya, hufanya kazi kwa muda mrefu,hupata ujira mdogo, hudhalilishwa na kunyanyaswa kijinsia na wengine hulazimishwa kufanya mapenzi bila ridhaa yao. Hayo ndiyo maisha ya kawaida kwa wafanyakazi hawa wa mashamba ya maua.
Ukiwa nje ya mashamba haya utavutiwa sana kuyaona make yanapendeza jinsi yalivyojegengewa, kama ujawai kuyaona,utadhani ni viwanda vikubwa vikubwa vya kuzalisha Nyuklia au ni viwanda vya nguo. Ukiyasogelea utapenda kuyasogelea zaidi, ndipo utakapoona watu wakiwa ndani ya nyumba ndefu iliyotengenezwa kwa karatasi za nailoni kwa kimombo nyumba hiyo inaitwa(Green house)yaani nyumba nyeupe. Kazi ya nyumba hii ni mahali ambapo maua hupandwa ndani, utajiuliza mbona sisi maua yetu yako nje ya nyumba. Sasa maua haya hupandwa ndani ya nyumba hii (Green house)kazi ya hii nyumba hasa, ni kudhibiti na kuruhusu mwanga na hewa vinavyoitajika kwenye maua na vinginevyo. Hivyo wafanyakazi wa maua huwa ndani ya hii nyumba nao wakigombania hewa,mwanga na maua ambayo upitia au kuruhusiwa kupita kwenye Green house.
Maua haya hupigwa Dawa kali za kemikali ili wadudu wasiyashambulie maua hayo ambayo, uwekewa mbolea mbali mbali za yabisi na maji, vyote hivi hufanyika ndani ya Greenhouse au nyumba ya kijani, ambamo wafanyakazi nao huwa ndani ya nyumba hii. Ebu pata picha kwanza,uko ndani ya nyumba yenye Dirisha moja dogo nyuma umepiga sumu kuua mbu au mende, je utaweza kukaa humo ndani na kuendelea kufanya kazi zako kama kawaida. Sasa kwenye mashamba haya au nyumba hizo yaani Green house mabo huwa hivyo, Dawa hupigwa wakati wafanyakazi wakiwa ndani katika maua.Sasa kinachofanyika huwa wafanyakazi wanahama kila mpiga Dawa anapowafikia.Yaani mpiga Dawa akifika unakofanyia kazi inabidi uhamie kule alikotoka kupiga Dawa. Kumbuka hawa watu wako ndani ya nyumba ndefu Green house, sasa cha kuogopesha zaidi wakati wa mambo yote haya ya upigaji wa madawa na uchumaji wa maua wakifanyika kwa wakati mmoja wafanyakazi wa haya mashamba ufanya kazi zao bila vifaa vya kufanyia kazi. Vifaa kama glove,makisi,yaani vivaa vya kuvaa mikononi na usoni au puani.
Sasa juzi nilitembelea mashamba haya niliyoyakuta ni zaidi ya niliyokuwa nayafahamu. Kulingana na maelezo ya wafanyakazi hao. Katika kipindi cha msimu mkuu au high peek wanavyokiita wao,ambacho uwa ni kipindi cha kuanzia mwezi wa kumi mpaka mwezi wa Tatu na kipindi cha valentine (Siku ya wapendanao).Wafanyakazi hao ufanya kazi masaa,kumi na manane 18,kuanzia saa kumi na moja 11 mapambazuko mpaka saa tano usiku bila kulipwa muda wa ziada (Overtime).Mbali na kurudi usiku, Hakuna usafiri unaotolewa kwa wafanyakazi wakiwemo wanawake na wasichana ambao wamejikuta mara kwa mara kwenye hatari ya kubakwa.
Idadi kubwa ya wafanyakazi hao ni wanawake ambao ni zaidi ya asilimia sitini (60%),Hawa wamejikuta kwenye Hatari hasa ya kukosa kizazi (Watoto)kwa sababu ya madawa yanayotumika kwenye mashamba hayo. Katika uchunguzi wangu, niliweza kupata maelezo ya mshahara kima cha chini mpaka juu. Katika mashamba haya wafanyakazi ulipwa mshahara kuanzia sh 30,000 mpaka wastani wa sh 75,000 kwa mwezi, na Hakuna ongezeko la mshahara. Labda uamue kuamia kwenye shamba jingine lenye maslahi zaidi kidogo. Mbali na mshahara mdogo Hakuna marupurupu yoyote ambayo mfanyakazi huyapata.
Wanawake nilioongea nao walinieleza kuwa,wamejikuta hata wengine siku zao za Hedhi hazionekani hata kama hawana mimba, kwa sababu ya Hadhali za madawa walinieleza katika mashamba haya hakuna hata Zahanati ya kutoa huduma ya kwanza pale ambapo mfanyakazi hutadhulika na madawa hayo,mbali na kwamba watu (Wafanyakazi­)wanadhulika mara kwa mara mpaka wengine kupoteza maisha na wamiliki wa mashamba haya au Selikali .
Uzalishaji na unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake unaofanywa na wasimamizi wa mashamba haya na wakati mwingine wafanyakazi wenzao wa kiume umekithili kwenye mashamba haya. Wakati mwingine wamejikuta wakisimamishwa kazi kama wakikataa kufanya nao mapenzi. Hiki ni kitu ambacho hufanyika kila siku,Bila vyombo vya Dola kujua. Katika mashamba mengine wanawake/wasichana huficha kusema kama wana mimba ili wasije wakafukuzwa kazi kabla ya Maternity leave.Wakati mwingine wanaamua kutoa mimba pindi pale wanapogundua kuwa Baba wa mtoto hajulikani au niwakutatanisha. Hapo wasichana wanaona ni bora kutoa mimba na haya ni ya kawaida kwenye mashamba haya.
Katika Arusha mashamba haya ya maua yamekua haraka sana katika miaka 10 iliyopita yakichangia Asilimia 15 za pato la mkoa kwenye fedha za kigeni yakiwa ya Tatu nyuma ya utalii na madani. Mavuno yake, yameongezeka kwa kipindi cha miaka mitano 5 kutoka tani 15,000 mpaka tani 30,000 kwa mwaka. Yakiongeza na kuleta mamilioni ya fedha kwenye nchi. Mbali na uongezekaji yake Hakuna faida yoyote wanayoipata wafanyakazi na wananchi wanaozungukwa na mashamba hayo, matokeo yake ni utumwa mkubwa walionao. Ukiangalia mikono ya wafanyakazi hasa ya wanawake ambao ushughulika zaidi na kukata na kufunga maua,lazima utokwe na machozi. Mikono imebadilika rangi,mwingine kucha hamna,uso umebabuka,lakini cha kushangaza hata Serikali ya Kata wanamofanyia kazi imenyamaza kimya kana kwamba hawajui kinachoendelea. Ebu jiulize ingawa, Hata Baadhi ya viongozi wengine wa chama na Serikali, watoto wao wanafanya kazi kwenye mashamba hayo lakini wamekaa kimya kila mmoja akiogopa kuwa wa kwanza kulisema. Ingawa mimi nimelisema ila mimi siogopi make nimeishaamua kuingia kwenye ulingo wa mapambano ya kuwatetea wanyonge kwa kutumia kipaji changu cha kuandika nilichopewa na mwenyenzi Mungu. Ningekuwa mwanasiasa ningepitia siasa ila mimi sio mwanasiasa. Basi napitia kwenye karamu.
Cha kushangaza kabisa tena sema kwenye mashamba haya hata vyama vya wafanyakazi vimenyamaza kimya kana kwamba tatizo hili hawalijui. Wafanyakazi hawa wa mashamba hawajui haki na majukumu yao kwenye vyama vya wafanyakazi Makampuni mengine yamenda mbali hata kufikia hatua ya kuwakataza wafanyakazi wao kutoshiriki au kutokujiunga na chama chochote cha wafanyakazi cha kushangaza zaidi nikwamba zaidi ya Asilimia 80% ya wafanyakazi wa mashamba hayo, Hawana ajira ya kudumu, wengi wao wanafanya kazi kama vibarua licha ya kwamba wamefanya kazi hapo zaidi ya miaka mitano. Ingawa wafanyakazi hao wameishapeleka malalamiko yao kwa mkuu wa Mkoa tangia mwaka jana Hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na Serikali dhidi ya wamiliki hao wa mashamba.
Ndani ya mashamba hayo,kuna mambo mengi wanayofanyiwa wafanyakazi hao, kama kupigwa mpaka kufa kuachiwa mbwa wawangate wafanyakazi,madawa makali yanayopigwa kwenye mashamba yanayofikia hatua ya kuwalewesha wafanyakazi, wakati mwingine kwenda kufia majumbani mwao bila Serikali kujua.
“Ni hatari tupu na tunafanya kazi, sasa wewe Bosi niambie tunafanya nini?” Aliuliza mama mmoja niliyekutana naye akitoka kazini uku akiwa amebeba mtoto mgongoni. “Sasa nahuyu mtoto naye anaingia kwenye nyumba hii Green house?” Niliuliza. “Sasa atakaa wapi?”alijibu na haya madawa hayamdhuru? Niliuliza, akijibu “mapenzi ya Mungu ingawa sio mara kwa mara nakuja naye”.Ebu fikilia huu ni uwekezaji au ni utumwa mwingine tumewaletea wananchi wetu. Mashamba mengine huku Arusha yamezungushiwa na nyaya za umeme, Ebu fikiria watoto wakisogelea itakuwaje? Kuna sehemu nyingine wazungu hawa(Wakulima wa mashamba ya maua)walitaka kuamsha shule. Eti iko kwenye mashamba yao. Wengine wamewazuia wananchi kuchota maji kisa Eti maji yako Mashambani mwao, walichokifanya kuwahi ni kuweka uzio wa umeme. Utumwa huu mashambani umekidhili mpaka unawalazimisha wasichana wadogo wanaofanya kazi mashambani humo kutoa rushwa ya ngono. Msichana lazima atoe rushwa ya ngono. Kila siku tunasema Rushwa ya ngono maofisini nenda mkafanye research kwenye mashamba ya maua mkaone. Namalizia kwa kusema kuwa utumwa umekithiri kwenye mashamba ya maua Arusha.

Thursday, May 04, 2006

YUPI KIONGOZI BORA WA UMMA?

Katika nyanja hii ya uongozi kuna kiongozi bora,mwaminifu kutoka kwa watu ambaye yuko tayari kufanya kai kwa manufaa ya umma. Na ubora huo wa uongozi sio huo wa kuongea tu, bali ni wa vitendo. Kiongozi wa umma ni yule anayetumia busara na upeo alivyopewa na mwenyezi Mungu kuwashauri na kuwasaidia watu kuelewa matatizo yao pamoja na sera za maendeleo, kwa kutumia Hoja za kimsingi. Watanzania wa leo si watu wakupewa Takrima.,Bakishishi, au sherehe, Hawapendi propaganda na ahadi kubwa zisizotekelezeka na Hawapendi kusikiliza viongozi wao wakilumbana na kutupiana lawama kuhusu matatizo yanayoikumba jamii.

Viongozi wa umma na hii ikijumuisha kila kiongozi lazima aonyeshe kufanya kazi kwa vitendo na kwa maneno. Wakati mwingine lazima tukumbuke kuwa kiongozi hawezi kufanya kila kitu kwa watu wake. Kiongozi anaweza kutoa muongozo mwelekeo au dira na jinsi gani watu waendeshe nchi yao wenyewe.Kiongozi wa umma hapaswi kuwa anatoa haadi ambazo hazitekelezeki au kukaa na kuanza kulaumiana lazima kiongozi anayeelewa matatizo waliyonayo Watanzania na atoe muelekeo na Muongozo ulio bora kwao ili waondokane na haya matatizo.

Hili ni jambo la muhimu, Kiongozi lazima aelewe na kufahamu ukweli wa matatizo tuliyonayo na aonyeshe kwa umma, kwa kutumia Nguvu zake ni jinsi gain Tanzania ya leo itaweza kuondokana na umasikini huu na kuwa nchi yenye neema. Kiongozi kama kiongozi haina maana kujidanganya kwa jambo Fulani Hasa umasikini kuwa haupo au kiongozi kujisifu mbele ya wapiga kura eti amepandisha bei ya kahawa, pamba., korosho nk. Kiongozi lazima aelewe kuwa matatizo yetu hayawezi kuisha kwa kujifanya na kuamini kuwa hayapo au kwa sababu tunawalaumu watu Fulani kuwa chanzo cha matatizo.

Viongozi lazima waelewe kuwa Hawawezi kuendesha nchi kwa kulalamika lalamika kuwa sisi ni maskini au Bei ya kahawa imeshuka, haisaidii ni sawa na kulalamika kuwa mvua haikunyesha. Kiongozi bora lazima ajue kuzitambua na kuzielewa alama za nyakati hizi, hata kama ziko nje ya uwezo wake, lazima ajue ni jinsi gain ya kuyatatua matatizo yanayotokea au kujitokeza nyakati hizi.Kiongozxi lazima ahaakikishe mipango ya Taifa inatekelezwa kwa kutumia akili aliyopewa na Mwenyezi Mungu. Hakuna njia nyingine, wala hakuna njia ya mkato.

Watanzania ni masikini na huu ndo ukweli wa mambo. Na ni tabia ya mwanadamu yeyote kuona utajiri na bahati alivyonavyo mwenzake kuliko yeye. Haipaswi kuwa kazi ya Kiongozi wa Tanzania kuwarubuni na kuwashawishi watu kuchukiana wao kwa wao kwa kisingizio za mali walizonazo. Wakati huo huo lazima ieleweke kwa umma na viongozi wetu kuwa Hakuna kiongozi anayepaswa kutumia madaraka yake vibaya ili kujipatia mali.



Kiongozi lazima afahamu kila kipato anachopata lazima kipatikane kihalali kama malipo yake kuto kwa umma, kwa kazi anayoifanya. Hii haitoshi kiongozi lazima aonyeshe ni jinsi gain ya kuendeleza nchi na watu wake. Mfano kama wawindaji kumi waliokamata sungura mmoja itakuwa ni ujinga na upotezaji wa muda kama watasitisha uwindaji. Na kuanza kugombania mgawanyo wa nyama wa sungura huyo mmoja. Lakini watakuwa wanafanya vizuri na Busara kama watatafuta mbinu na njia mpya za uwindaji ili kujiongezea wingi wa nyama, Na hii ni sawa na Viongozi wa Tanzania. Hii ni nchi Masikini, nchi isiyozaa matunda ya kumtosheleza kila Mtanzania ili aishi maisha bora , Tunafanana na wawindaji kumi wenye sungura mmoja katikati yao, hatuna njia ya kuondikana hili .Hii aina maana kuwa serikali iongeze pesa nyingi kwenye mzunguko wa uchumi . Kama kiongozi mmoja wa chama cha siasa aliyekuwa anatumia falsafa ya kuwajaza watu mapesa . Kuongeza fedha nyingi kwenye uchumi wa nchi ni kuongeza mfumuko wa bei kwenye nchi jambo ambalo litaharibu uchumi wetu na hili ni bora kila kiongozi akalielewa.

Haina maana kiongiozi kuelewa Takwimu kabla Hajatambua kuwa Tanzania ni masikini . Tena ya kutupwa. Tunaona na tunaishi na umasikini , wakati mwingine viongozi uchanganya mambo kwa kutazama watu wachache wanaoendesha magari yao binafsi au kwa takwimu zinazotolewa na waziri wa fedha wakati wa kipindi cha Bajeti Bungeni, na kuamini kuwa nchi yao ni tajiri na kwamba umasikini tulionao ni kutokana na mgawanyo mbaya w rasilimali au ni unyonyaji,wakati mwingine kuamini kuwa umasikini hamna kabisa, kama kiongozi mmoja wa juu kwenye Serikali ya awamu ya tatu aliyesema hakuna Mtanzania yeyote anayeweza kukosa kupata shs 500/= kwa siku. Sina maoni kuwa mgawanyo wa utajiri wa nchi hauna maana la asha, una maana sana Hasa kwa watu kama sisi tunaamini na kukubali azimio la Arusha kuwa lazima pawepo na mgawanyo sawa wa mali ya umma. Ni sawa na wale wawindaji kumi wenye sungura mmoja katikati yao, lazima tutafute njia ya kuongeza pato la taifa sisi wenyewe tukitaka haya yote yatimie, lazima tusimamishe upandishaji wa mishahara ya vigogo serikalini na tuongeze mishahara ya wafanyakazi wa kima cha chini.

Lazima tuimarishe vyama vya ushirika ili kupunguza unyonyaji wa madalali kwa mkulima mdogo , ni lazima tutafute njia mbadala na mfumo mpya wa kilimo tuondokane na kilimo cha Jembe la mkono tuamie kwenye matumizi ya trekta , lazima serikali ipambane na makampuni yananyotengeneza na kuwauzia wakulima mbegu zisizofaa serikali lazima iongeze ruzuku kwenye pembejeo za kilimo.
Kila kiongozi lazima aelewe kuwa watanzania walio wengi wataendelea kuishi vijijini,mahitaji na maisha yao yote yatategemea kilimo. Hii ina maana kuwa lazima kilimo chetu kiwe cha kisasa na ni lazima tuimarishe vyama vya ushirika ili kuwawezesha wakulima wetu wawe na akiba kidogo ya kuhifadhi, na ni jukumu la serikali kuakikisha kuwa inawasogezea wakulima hawa Benki karibu. Tukiwasogezea Benki karibu wakulima Hawa kama vimebaki vihela vyao, hivyo vlivyosalia bada ya kununua vitu dukani au labda baada ya kununua Ngo’mbe au ameongeza mke wa pili na bado kuna kaakiba kadogo , kama Benki iko karibu anaweza kuviweka vipesa vyake hivyo akiba.Mkulima akiweka akiba yake Benk anachohitaji ni usalama tu wa vile vihela yvake, Hatafuti kuzaa. Kila kiongozi wa umma lazima hayo hayafahamu.

Na mimi nayataja hivyo ili kusudi viongozi wa serikali ambao wanaamini na kusadiki ushauri unaotolewa na Benk ya Dunia na mashirika yake, na wale wanaoamini kuwa uchumi wanchi utayumba kwa sababu kiongozi au viongozi wa Umma watakataa masharti mazuri ya mashirika hayo, sio kweli.Mashirika haya ya Kimataifa yanapotosha na kutuyumbisha, lazima viongozi wetu mkatae, naeleza makusudi muelewe mambo mengi ya mashirika haya ya Kimataifa (IMF na wenzake). Hayana chembe ya utaalamu ndani yake, ni udanganyifu mkubwa. Ebu fikiria ni kiongozi gani wa Benk ya Dunia aliyewahi kufika Singida au Kigoma na kuweza kuyaona matatizo ya wananchi wa Mikoa hii angalau ata kwa dakika tano tu. Jiulize maendeleo ya Ulaya au nchi zote za magharibi yametokana na mashirika haya? Nasema ili kila kiongozi mwenye uchu wa maendeleo ya Mtanzania ajue. Kuwa haina maana, kwamba kabla hatujapandisha bei ya umeme twende kuyaomba mashirika haya yaturuhusu na ina maana kuwa mipango yetu ipitie kwenye mashirika haya; nakataa kata kata.

Mashirika haya na vibaraka wa mashirika haya wanaamini kuwa nchi inaweza kuendelea na kumiliki maendeleo yake bila wananchi wake kumiliki njia na mchakato mzima wa uzalishaji mali wakati duniani kote na katika vitabu vya uchumi, nani anamiliki nini ni swali na suala la msingi kwenye nchi husika. Uku mashirika haya yakiendelea kutupotosha, viongozi wetu na wananchi tunazidi kuonyesha.“qui tacet concentive viditur” kimya means ndiyo au tunakubaliana nayo.

Katika mchakato mzima wa kuonyesha na kuelekeza ni yupi kiongozi wa Umma, na ni mkondo gani Taifa lifuate. Sijawasahau waandishi au watu wenye taaluma ya habari bila kuwasahau wanaomiliki vyombo vya habari, kwanza kabisa nawapongeza sna kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuelimisha, na kuburudisha jamii ya Tanzania ambayo ni maskini. Make nisipowapongeza nitakuwa mchoyo wa pongezi kama wahaya wanavyosema “Entasima Ekalya omutima gyemanzi”

Tanzania tumepiga hatua kwenye uhuru wa vyombo vya habari.Lakini najiuliza Je uhuru wa vyombo vya habari ni msingi wa kubomoa na kuaribu kabisa utamaduni wa Mtanzania? Mimi sidhani kama ni kweli uhuru wa vyombo vya habari ni kuaribu utamaduni wanchi. Leo hii, kama viongozi wa umma tumekubali watanzania wazamishwe kwenye habari za umbeya, udaku, ngono na majungu. Tanzania leo tuna magazeti na majarida ya umbea kuliko nchi nyingine yoyote barani Africa. Utasikia Fulani kapata buzi!!!, Oho Fulani kafumaniwa magomeni, oho kigogo (kiongozi) akutwa gesti ……n.k. Ebu jiulize kama waandishi wa habari na wamiliki wa vyombo vya habari wanawatengenezea kizazi cha leo na cha kesho ufahamu gani? Waandishi na wamiliki wa majarida haya, na viongozi wetu wanatakiwa wajue kwamba anayeamua juu ya maitaji ya jamii kwenye habari ni jamii yenyewe na wala sio wao. Ukiwauliza watakwambia ni kwenda na wakati msemo unaotumika kuhalalisha mabaya kuwa mazuri, siku hizi tunavaa nguo fupi, na zisizofaa eti; tunakwenda na wakati. Je huo wakati tunaenda nao uko uchi? Au sisi tunaulazimisha uwe uchi. Zamani ndo watu waliishi utupu, sasa sisi leo tunaojidai kusonga mbele kwa kuvaa nguo nusu uchi, uku ni kurudi zamani na wakati, sio kusonga mbele au kwenda na wakati.
Kiongozi yeyote anayejijua kuwa yeye anapaswa kutumikia umma wa Taifa la Tanzania. Taifa lenye umaskini sana, Taifa ambalo watu wake ni wapole watulivu kuliko Taifa lolote barani afrika, Taifa ambalo watu wake wamezoea kuonyeshwa punda na kuambiwa ni ng’ombe; mbuzi na kuambiwa ni ngamia, watu ambao viongozi wao wamezoea kuwaambia kuwa ni wavivu wa kufikiria. Sasa ni wajibu wa kila kiongozi na mdau wa maendeleo ya Tanzania kujua kuwa ni viongozi na wale wenye mamlaka na wajibu mkubwa wa kuendeleza jamii na sio kujipatia manufaa na upendeleo. Kama kweli mtayazingatia haya niliyojaribu kuwaeleza nadhani huu utakuwa mwanzo mzuri wa “Taifa letu kuelekea kweye neema ya kila Mtanzania”.Mungu ibariki Africa,Mungu ibariki Tanzania.